Msumba News Blog
Blog hii inajihusisha na machapisho ya kuhabarisha,kuelimisha na kuburudisha.
15/07/2026
*NAIBU SPIKA SILLO AUNGANA NA WANANCHI MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU.*
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ameungana na wananchi kuupokea Mwenge wa Uhuru uliowasili leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ukitokea Wilaya ya Kiteto.
Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang'onda, Sillo amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupeleka fedha nyingi katika Jimbo la Babati Vijijini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema uwekezaji huo umewezesha utekelezaji wa miradi katika sekta muhimu zikiwemo elimu, afya, maji, barabara na huduma nyingine za kijamii, hatua ambayo imeendelea kuharakisha maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Sillo amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang'onda, ameendelea na ratiba ya kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 inasema: "Tanzania ni Yetu Sote, Tushik**ane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."
11/07/2026
GAVANA TUTUBA AIPONGEZA IAA KWA KUWAJENGA VIJANA KUJIAJIRI
Na Mwandishi Wetu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ameipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa juhudi zake za kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia Kituo chake cha Kiatamizi cha IAA Business Start Up Centre, kinachowasaidia kubadili mawazo ya kibunifu kuwa biashara zenye mafanikio.
Tutuba alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la IAA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema anafurahishwa na maendeleo ya kituo hicho, akieleza kuwa anakumbuka hatua za mwanzo za kuanzishwa kwake na sasa anashuhudia matokeo chanya kupitia vijana wanaobuni na kuanzisha biashara zinazochangia maendeleo ya uchumi.
"Ninakumbuka tulipoanzisha kituo hiki. Leo ninafurahi kuona kinaendelea kuzalisha vijana wenye ubunifu na kuwageuza mawazo yao kuwa fursa za kiuchumi," alisema Tutuba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa, Uhusiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, alisema taasisi hiyo imeendelea kuwekeza katika kuwaandaa vijana kwa kujiajiri kupitia Kituo cha Kiatamizi, sambamba na kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Alisema mbali na mafunzo ya darasani, IAA imeweka mazingira rafiki yanayowezesha wanafunzi kuanzisha biashara zao huku wakipata ushauri wa kitaalamu, mafunzo ya ujasiriamali na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mawazo yao yanakua na kuwa biashara endelevu.
Sarah alisema katika mwaka wa masomo 2024/2025 zaidi ya vijana 8,600 walinufaika na programu za ujasiriamali, huku vijana 1,520 wakiwasilisha mawazo mbalimbali ya biashara kupitia kituo hicho.
Aliongeza kuwa kati ya mawazo hayo, zaidi ya biashara 50 zilianzishwa na kampuni 12 zikafanikiwa kusajiliwa rasmi, zikijikita katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, teknolojia, sanaa, uhifadhi wa mazingira na shughuli nyingine za kiuchumi.
Alisema kupitia Kituo cha Kiatamizi, wahitimu wengi wamefanikiwa kujiajiri na wengine kuanzisha kampuni zinazowaajiri vijana wenzao, hatua inayochangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu na ujasiriamali.
04/07/2026
*MJI WA SERIKALI MTUMBA KUWA MFANO WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KUPITIA GESI ASILIA*
Imeelezwa kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya kuufanya Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kuwa mfano wa matumizi ya nishati safi kupitia mradi wa usambazaji wa gesi asilia.
Miundombinu hiyo itaunganisha gesi asilia katika majengo ya Wizara, ofisi za Ubalozi, taasisi za Serikali, majengo ya biashara, hoteli, migahawa pamoja na makazi ya eneo la Mtumba.
Hayo yameelezwa na Mjiolojia kutoka Wizara ya Nishati, Nuru Helambili wakati akitoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda la Wizara ya Nishati katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Helambili amesema mradi huo unalenga kujenga kituo cha kupokelea gesi (Gas receiving terminal) itakayokuwa ikisafirishwa kwa magari maalum kutoka Kituo Mama cha CNG kilichopo Mlimani City, Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa mradi huo utahusisha pia ujenzi wa kituo cha kupunguza mgandamizo wa gesi, mtandao wa usambazaji na kituo cha kujazia gesi asilia kwenye magari.
Helambili ameeleza kuwa katika mwaka 2026/2027 Serikali itakamilisha tathmini ya athari kwa mazingira na jamii na kuanza taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likitenga shilingi bilioni 14.40 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo.
04/07/2026
RAIS SAMIA KALETA BILIONI 1.2 ZA UJENZI WA SHULE ZA MSINGI MLIMBA- PROF. SHEMDOE
• Akagua miradi ya maendeleo, ahimiza ikamilike kwa wakati
Na OWM - TAMISEMI, Mlimba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu, amewaletea wananchi wa Mlimba kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2 za kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za msingi zitakazoongeza fursa za elimu na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Prof. Shemdoe amesema hayo Julai 3, 2026 katika Uwanja wa Tandare, Kata ya Igima, wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji wa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
"Leo nimekuja na habari njema kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaletea Shilingi
Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa Shule za Msingi Mgeta na Nganyangira. Nimejiridhisha kuwa fedha hizo tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya halmashauri ili utekelezaji uanze mara moja," ameeleza Prof. Shemdoe.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe amezindua mabasi mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, amefungua Shule ya Msingi Ngajengwa na kukabidhi vipaza sauti kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi katika maeneo yao.
Aidha, Prof. Shemdoe amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba saba za watumishi, kukagua ujenzi wa wodi mbili za upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, pamoja na kutembelea barabara inayojengwa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi.
"Nimetembelea daraja kubwa linalojengwa katika Kata ya Mgeta ambalo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wake. Vilevile, kuna daraja lingine limepatiwa
Shilingi Bilioni 1.7. Huu ni uwekezaji mkubwa unaoonyesha dhamira ya Mhe. Rais ya kuwaletea wananchi maendeleo," amesema Prof. Shemdoe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima amesema Wilaya ya Mlimba ndiyo kinara wa uzalishaji katika mkoa huo, huku akibainisha kuwa mapato ya halmashauri hiyo yanaendelea kuongezeka kwa kasi kuliko halmashauri nyingine kutokana na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji na ukusanyaji wa mapato.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Mhe. Dkt. Kellenrose Rwakatare amesema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya shule, ikiwemo kukamilisha majengo yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, hatua inayochangia kuwapatia wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia.
03/07/2026
WAZIRI DKT AKWILAPO AKUTANA NA TAASISI YA WAPIMA ARDHI TANZANIA.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania (IST), ambapo pande hizo zilijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya Upimaji Ardhi na sekta ya ardhi nchini.
Ujumbe wa IST ulioongozwa na Rais wa taasisi hiyo, Dkt. Julian Magezi Ijumulana na Upande wa Wizara ya Ardhi uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Upimaji Ardhi ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor, ulimtembelea Waziri Dkt. Akwilapo kwa lengo la kujitambulisha.
Aidha, ujumbe huo ulimuelezea Mhe Dkt Akwilapo mikakati ya taasisi hiyo, ikiwemo maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 45 ya kuanzishwa kwake pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka unaotarajiwa kufanyika Novemba 2026 katika Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza katika kikao hicho, Julai 2, 2026 jijini Dar es Salaam Dkt. Akwilapo alisema ameyapokea mawazo na mapendekezo yaliyowasilishwa na Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi kwa kuzingatia maslahi ya sekta ya ardhi na maendeleo ya nchi.
Aidha, Waziri Dkt. Akwilapo alisisitiza kuwa swala la sheria ya Upimaji ardhi sura 324 na usajili wa Wapima ardhi sura 270 amelipokea na atafanyia kazi kwa haraka kwani Wapima Ardhi wana nafasi muhimu katika kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi nchini kupitia upimaji sahihi.
03/07/2026
TARURA YAIMARISHA MPANGO WA CBRM KUBORESHA MATENGENEZO YA BARABARA NCHINI.
Mpango wa Matengenezo ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (Community Based Routine Maintenance – CBRM) unaotekelezwa na Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) utasaidia kuondoa hoja mbalimbali na kuimarisha upatikanaji wa vikundi vya kijamii katika matengenezo ya kawaida ya barabara nchini.
Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira na Jamii, Dkt. Haledeus Makene wakati akifungua mafunzo ya mpango huo kwa Menejimenti, Mameneja wa Mikoa na Maofisa Ununuzi wa TARURA kutoka mikoa mbalimbali yanayofanyika jijini Mwanza.
Dkt. Makene amesema kuwa uundwaji wa vikundi hivyo utaleta mafanikio makubwa kwa Wakala huo na Serikali kwa ujumla kutokana na wanufaika wake kuwa wakazi wa maeneo husika hali inayowawezesha kumiliki na kulinda miundombinu inayowazunguka.
Amesema hatua hiyo itachangia barabara nyingi zinazosimamiwa na TARURA kupitika misimu yote kwani wananchi wenyewe watawajibika kuzitunza.
"Tunahitaji wananchi wenyewe wamiliki barabara zilizopo katika maeneo yao. Vikundi vinavyoundwa vitatoka katika maeneo yao na kufanya matengenezo ya kawaida mara kwa mara, hivyo kuwa walinzi wa miundombinu pia kuongeza kipato na kuinua hali zao kiuchumi", amesema Dkt. Makene.
Kwa upande wake, Mratibu wa CBRM, Mhandisi Richard Missa amesema mpango huo wa miaka mitatu unatarajiwa kutekelezwa katika halmashauri 70 zilizopo kwenye mikoa 25 ukiwa na lengo la kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa takribani kilomita 15,000.
Hata hivyo, Mhandisi Missa amesema tangu kuanza kwa mpango huo kilomita 7,000 tayari zimefikiwa.
Amesema moja ya majukumu ya TARURA ni kuhakikisha barabara zinapitika mwaka mzima hivyo vikundi hivyo vinapaswa kufanya kazi za kufyeka nyasi, kusafisha na kufungua mitaro ya maji pamoja na matundu ya makalavati ili hata wakati wa mvua miundombinu iwe salama na isilete uharibifu.
Naye, Mratibu wa Kitaifa wa Programu kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Dampu Ndenzako ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kushirikiana katika kujenga uwezo wa utekelezaji wa mpango huo hatua inayolenga kuleta mageuzi katika upitikanaji wa barabara mwaka mzima pamoja na kuwaongezea kipato wana kikundi.
03/07/2026
PROF. SHEMDOE AMSHUKURU RAIS SAMIA NA BARRICK KWA KUPELEKA TABASAMU MASHULENI
• Aitaka k**ati iliyoshiriki majadiliano ya awali kujadiliana tena
Na OWM - TAMISEMI, Kibaigwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals kwa kupeleka tabasamu mashuleni kupitia majadiliano waliyoyafanya ambayo yalipelekea Barrick kuchangia zaidi ya shilingi bilioni 70 za kitanzania ambazo zimewezesha ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule za sekondari 132 nchini.
Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo kwa Mhe. Rais na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals Julai 02, 2026 akiwa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa miundombinu ya shule za kidato cha tano na sita, ambao unaofadhiliwa kupitia ushirikiano wa Serikali na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals.
“Nampongeza sana Mhe. Rais kwa kuwaona Barrick k**a wadau muhimu, na nawashukuru na kuwapongeza Barrick kwa kuleta fedha za kuwekeza kwenye sekta hii muhimu ya elimu,” ameeleza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, ni chini ya uongozi makini wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndipo yalipoanzishwa majadiliano kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick ya kuimarisha ushirikiano katika kuchangia maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji wa sekta ya elimu, na kuongeza kuwa majadiliano hayo yalipelekea kupatikana kwa zaidi ya bilioni 70 za kitanzania ziloizotumika kwenye ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo.
Aidha, Prof. Shemdoe ameelekeza k**ati iliyoshiriki kwenye majadiliano ya awali ya mwaka 2023 na Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals kurejea tena kwenye majadiliano mengine na kampuni hiyo, ili awamu awamu ya pili ya mradi huo ikikamilika zipatikane fedha nyingine za kuendelea kujenga miundombinu bora ya elimu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Barrick - Twiga Minerals Bi Penina Kituku ambaye ni Meneja wa Fedha amesema kuwa, uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 70 za kitanzania walioufanya una maana kubwa kwa jamii na unakwenda moja kwa moja kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, ikiwa ni pamoja kutoa fursa kwa wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia elimu Bw. Atupele Mwambene,amesema kwamba mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri ambao wanajiunga na kidato cha tano, na kuongeza kuwa afua ambazo zimetekelezwa nchi nzima mpaka hivi sasa ni ujenzi wa madarasa 1090, mabweni 270 na matundu ya vyoo 1640.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kibaigwa, Bw. Alex Sailemi amesema kuwa, wakazi wa Kibaigwa wanayo sababu ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Kampuni ya Barrick kwa kujengewa miundominu ya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, DKT. FLORENCE SAMIZI: SERIKALI KUIBORESHA SEKTA YA AFYA BAGAMOYO; AAHIDI MAOMBI YA SUBIRA MGALU KUFANYIWA KAZI
Bagamoyo, Julai 2, 2026 – Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amepokea na kuahidi kuyafanyia kazi maombi muhimu yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. CPA Subira Khamis Mgalu, yanayolenga kuboresha huduma za afya na kuendana na kasi ya maendeleo ya Wilaya ya Bagamoyo.
Dkt. Samizi amewasili Bagamoyo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shaibu Issa Ndemanga, kabla ya kukagua Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bagamoyo pamoja na kufanya ziara katika Hospitali ya Wilaya.
Mhe. Mgalu amesema kutokana na Bagamoyo kukua kwa kasi na kuelekea kuwa mji wa viwanda pamoja na kupokea miradi mikubwa ya kimkakati, kuna umuhimu wa Serikali kuanza mipango ya kujenga hospitali kubwa zaidi, kukamilisha jengo la upasuaji na kuongeza magari ya wagonjwa (ambulance) ili kuboresha huduma za rufaa.
Akijibu maombi hayo, Dkt. Florence Samizi amesema Serikali imeyapokea na itayafanyia kazi kupitia mipango yake ya maendeleo ya sekta ya afya.
Aidha, amempongeza Mhe. CPA Subira Khamis Mgalu kwa juhudi anazoendelea kuzifanya katika kutetea na kusimamia maendeleo ya wananchi wa Bagamoyo, akibainisha kuwa uzoefu wake katika uongozi ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi unaonekana kupitia namna anavyowasilisha vipaumbele vya wananchi.
Naibu Waziri pia amewataka viongozi wote kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini.
02/07/2026
*MAAFISA VIPIMO WAWATEMBELEA WAJASIRIAMALI SABASABA NA KUWAPA ELIMU YA VIPIMO*
*_DAR ES SALAAM_* - Katika siku ya tano ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), Julai 2, 2026, Maafisa kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wamewatembelea wajasiriamali mbalimbali na kuwapatia elimu ya vipimo.
Wakiongozwa na Meneja wa WMA Mkoa wa Ki-vipimo Ilala, Bw. Muhono Nashon, wataalamu hao wa vipimo wamewaelimisha wajasiariamali wadogo wadogo namna sahihi ya uandishi wa alama katika vifungashio vya bidhaa zao ili zikidhi vigezo vya soko la kimataifa, pamoja na masuala mengine muhimu kuhusu vipimo.
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa WMA, Bi Veronica Simba amesema ni mojawapo ya mbinu za kuwafikia wadau mbalimbali wa vipimo wanaoshiriki katika Maonesho hayo.
Aidha, ameongeza kuwa, hatua hiyo pia imelenga kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga ambaye awali alipotembelea Banda la Wizara pamoja na Taasisi zake, aliwataka watumishi hao kuwafuata wadau mbalimbali na kuwapatia huduma badala ya kusubiri wale tu wanaofika bandani.
Utaratibu huo umepongezwa na wajasiriamali waliofikiwa wakisema kuwa umewawezesha kupata elimu ya vipimo pasipo kulazimika kuacha mabanda yao kwenda katika banda la WMA kufuata huduma hiyo.
Utoaji elimu ya vipimo kwa wadau mbalimbali ni utaratibu wa kawaida ambao hutekelezwa siku zote na WMA k**a sehemu ya majukumu ya kazi.
*ULINZI NA USALAMA WA TAIFA LETU HAUNA CHAMA, DINI WALA KABILA - DKT. NYANSAHO*
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewataka wananchi wa Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa ulinzi na usalama wa taifa hauhusiani na chama cha siasa, dini wala kabila.
Dkt. Nyansaho ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Julai 2, 2026, wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Akimkaribisha Waziri Mkuu katika eneo hilo, Dkt. Nyansaho amesema Serengeti inapaswa kuwa mfano wa kudumisha amani, akieleza kuwa eneo hilo ni nyumbani kwake na hivyo linapaswa kuwa chanzo cha mshik**ano na utulivu.
"Waziri Mkuu, karibu nyumbani, lakini kwa namna ya kipekee sana. Hapa nyumbani ndipo chanzo cha amani kinapaswa kuanzia," alisema.
Amesema kuaminiwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akiwa mzaliwa wa Serengeti, ni heshima kubwa inayoweka wajibu kwa wananchi wa eneo hilo kuwa vinara wa kulinda amani ya taifa.
"Kwa sababu Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliniamini mimi ambaye natokea hapa Serengeti na kunipa jukumu la Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa maana hiyo ndugu zangu wa Serengeti, naomba sisi tuwe chanzo cha kuleta na kulinda amani," alisema.
Aidha, Dkt. Nyansaho amesisitiza kuwa ulinzi na usalama wa taifa ni jukumu la kila Mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.
"Ulinzi na usalama wa taifa letu hauna chama, dini wala kabila. Sisi k**a wananchi, usalama na amani ya nchi yetu ni jukumu la kila mzazi na kila mmoja bila kujali chama au dini," alisema.
Katika hatua nyingine, ametoa wito maalumu kwa wananchi wa Serengeti, Kanda Maalumu na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuwa mabalozi wa amani kwa kuhakikisha wanaendelea kuhimiza mshik**ano, umoja na utulivu ili kuendeleza maendeleo ya taifa.
Click here to claim your Sponsored Listing.
Category
Contact the business
Telephone
Website
Address
Arusha