Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea

Share

Ukurasa rasimi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 31/07/2026

WATUMISHI WA HOMSO WAKUMBUSHWA MAADILI NA SHERIA ZA UTUMISHI

Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea wamefanya kikao kazi cha kukumbushana kanuni, sheria na maadili ya utumishi wa umma. Mganga Mfawidhi Dkt. Magafu Majura amesisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kufuata miongozo ya kazi kwa uadilifu, nidhamu na ubunifu ili kutoa huduma bora kwa wananchi. “Tuwe mfano wa nidhamu na uzalendo kazini.

Hata hivyo kikao hicho kimetoa taarifa mbalimbali juu ya uendeshaji wa hospitali ikiwemo maboresho ya huduma, matumizi sahihi ya rasilimali na mipango ya kuimarisha miundombinu.”Ushirikiano na uwajibikaji ndio utakaotufikisha mbali katika kutoa huduma bora na endelevu.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 31/07/2026

ZAWADI ZA MATENDO YA HURUMA: POLISI RUVUMA WAJENGA DARAJA NA WANANCHI HOMSO

Wakati wengi huliona Jeshi la Polisi likitekeleza majukumu ya ulinzi na usalama, Julai 30, 2026 limeandika sura nyingine ya huduma kwa jamii baada ya kuwafariji wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Songea (HOMSO) kwa kuwapatia mahitaji muhimu kwao na watoto wachanga.

Msaada huo ulitolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani, kwa kushirikiana na Kitengo cha Polisi Jamii, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi kupitia matendo ya huruma.

Bidhaa zilizokabidhiwa zilijumuisha mahitaji muhimu ya akina mama na watoto wachanga, yakilenga kupunguza changamoto zinazowakabili familia katika siku za mwanzo baada ya kujifungua.

Hatua hiyo inaendeleza falsafa ya polisi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kijamii zinazogusa maisha ya wananchi, sambamba na jukumu lao la msingi la kulinda amani na usalama.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 30/07/2026

MGANGA MFAWIDHI ALISHUKURU JESHI LA POLISI KWA MATENDO YA HURUMA KWA WAZAZI NA WATOTO WACHANGA

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dkt. Magafu Majura ametoa shukrani kwa jeshi la polisi Mkoa wa Ruvuma kupitia kitengo cha usalama barabarani kwa kushirikiana na kitengo cha polisi jamii ngazi ya wilaya na mkoa, kwa mchango wao wa zawadi za matendo ya huruma kwa wagonjwa ambao ni wazazi na watoto wachanga waliolazwa hospitalini.

Akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo leo 30 Julai, 2026 hospitalini hapo, Dkt. Majura amesema kupitia matendo hayo ya huruma yameimarisha uhusiano baina ya wananchi na jeshi la polisi.

“Huu ni ushirikiano mzuri. Unatufundisha kuwa usalama na afya vinaenda pamoja,” amesema Dkt. Majura.

Ameahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa jamii yote ya mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Mrakibu wa Polisi (SP) Muya Maunganya Mkuu wa Kikosi Cha Usalama Barabarani Wilaya ya Songea amesema kutoa matendo ya huruma kwa wagonjwa wazazi na watoto wachanga ni mkakati wa kujenga uhusiano imara kati ya jeshi la polisi na wananchi.

“Sisi polisi ni sehemu ya jamii. Tunapowasaidia wazazi na watoto hospitalini tunaoonyesha upendo na huduma,” amesema Maunganya

Naye, Mrakibu MsaidiI wa Polisi (ASP) Melinda Mgumba Mkuu wa Polisi jamii Wilaya ya Songea amesema zawadi zilizotolewa kwa wazazi na watoto wachanga zitaleta imani kubwa kati ya wananchi na jeshi la polisi.

“Polisi tupo kwa ajili ya wananchi. Tunaposhiriki nao katika nyakati za furaha na shida, tunajenga imani na upendo,” amesema Mgumba.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 28/07/2026

WATU SABA WANUSURIKA KIFO BAADA YA SAA 27 NDANI YA MAJI YA ZIWA NYASA; RAIA WANNE WA UHOLANZI WAOKOLEWA SALAMA

Walipotea katikati ya mawimbi makali ya Ziwa Nyasa. Saa zikapita, matumaini yakaanza kufifia. Lakini baada ya takribani saa 27 wakiwa majini, watu saba, wakiwemo raia wanne wa Uholanzi, waliokolewa salama katika tukio lililogeuka simulizi ya ujasiri na mshikamano wa wananchi wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Majina ya manusura hao ni pamoja na
1. Hussein Ajalia Hasa
2. Shadrack Mpata
3. Filimon Moyo
4. Hendrika Verveda
5. Christian Gerlagh
6. Lente Maarjse
7. Mitchel Haring
Ajali hiyo ilitokea Julai 26, 2026, saa 4:00 asubuhi, wakati boti iliyokuwa ikitoka Bandari ya Mbamba Bay kuelekea Malawi ilipopata hitilafu ya injini, kujaa maji kutokana na dhoruba kali na baadaye kupinduka. Operesheni ya uokoaji ilifanikiwa saa 10:00 jioni Julai 27, 2026, ikiwaokoa manusura wote saba.

Akizungumza baada ya uokoaji, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, aliwapongeza wananchi wa Nyasa kwa ushirikiano wao mkubwa na kusisitiza umuhimu wa kufuata tahadhari za usalama na kuepuka safari za ziwani wakati hali ya hewa ni mbaya.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, manusura wote saba wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri. Tukio hilo linahusisha manusura saba, wanne wao wakiwa raia wa Uholanzi.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 21/07/2026

DKT. MAJURA AWATAKA WATAALAMU WA AFYA NA JAMII KUIBUA WAGONJWA WA HIMOFILIA KATIKA JAMII

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea DKt. Magafu Majura amewataka wataalamu wa afya na jamii kuwaibua wagonjwa wa Himofilia waliopo katika jamii na kuwaleta hospitali kwa ajili ya matibabu.

Wito huo, ameutoa leo tarehe 21/7/2026, wakati wa ufunguzi wa Kliniki ya Himofilia hospitalini hapo, amesema kuwaibua wagonjwa mapema kutasaidia kupunguza matatizo ya kutokwa na damu kupita kiasi na ulemavu wa viungo.

‘’Tutatumia nafasi ya ziada ili kutembele tasisi nyingine hasa shule kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa awali ili kuwabaini wenye viashiria mapema’’ amesema Dkt. Majura

Dkt. amesisitiza Kliniki hiyo itatoa huduma za upimaji, ushauri wa kitaalamu, matibabu na ufuatiliaji wa karibu kwa wagonjwa wote wa Himofilia mkoani Ruvuma na mikoa. Dkt. Majura amesema wahudumu wa afya, walimu na viongozi wa jamii kutumia fursa ya mafunzo waliyopata kuwa mabalozi wa kutoa elimu ili jamii ipate uelewa juu ya dalili na utambuzi wa ugonjwa huo.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania Bw. Abdallah Makalla amesema takwimu zinaonsha kwamba duniani kati ya watu 10,000 mtu mmoja anapatikana na ugonjwa wa himofilia. Na kwa Tanzani kulingana na idadi ya watu inakadiliwa kuwa na wagonjwa 6700 lakini kati ya hao ni wagonjwa 677 ndio wameweza kugundulika na zaidi ya asilimia 90 hawajagundulika.

Naye, Dominic Seye Mgonjwa wa Himofilia ameiomba serikali iweke mazingira rafiki kwa watoto wenye ugonjwa wa Himofili shule na watu wazima katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuwasaidia.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 20/07/2026

KUPITIA MAFUNZO, MGANGA MFAWIDHI AZITAKA KADA ZA AFYA NA JAMII ZIIBUE WAGONJWA WA HIMOFILIA

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea, Dkt. Magafu Majura amewataka washiriki wa mafunzo ya ugonjwa wa Himofilia watumie fursa hiyo kuwaibua wagonjwa wengine waliopo katika jamii na kuwaleta hospitali kwa ajili ya matibabu.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum kwa kada za afya, wahudumu wa tiba asili, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, waalimu, maafisa elimu, wagonjwa pamoja na wazazi. Uliofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea, leo 20/7/2026.

Amesema mafunzo ya ugonjwa wa Himofilia yataleta uelewa wa dalili, utambuzi wa mapema na namna ya kutoa huduma. Mganga Mfawidhi amesisitiza kuwa ukigundulika mapema ugonjwa huo unadhibitiwa na unapunguza matatizo ya kutokwa na damu.

Mara baada ya kufungua mafunzo hayo, DKt. Majura amesema 21/7/2026 kutakuwa na ufunguzi rasmi wa Kliniki ya Himofilia ndani ya hospitali hiyo. Kliniki hiyo itatoa huduma za upimaji, ushauri wa kitaalamu, matibabu na ufuatiliaji wa karibu kwa wagonjwa wote wa Himofilia mkoani Ruvuma.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania Bw. Abdalah Makalla amesema wanarajia kukaa kwa muda mrefu na hospitali, Waganga Wakuu na wafanyakazi wengine wa afya ili wapewe mafunzo ya kina kuhusu ugonjwa huo.

Makalla amesema lengo ni kuhakikisha watakapoondoka kwenye mafunzo hayo wawaache na uelewa zaidi wa namna ya kubaini, kutoa huduma na kutoa ushauri kwa wagonjwa na wazazi.

17/07/2026

FARAJA KWA WAZAZI MATEGE KWA WATOTO YATOLEWA HOMSO

Kitengo cha Viungo Bandia na Vifaa Saidizi kilichopo Idara ya Utengamano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea kina vifaa na wataalamu wenye uwezo wa kutengeneza na kutoa matege kwa watoto.

Huduma hii imelenga kuwasaidia watoto wenye changamoto za miguu kupata usaidizi mapema ili waweze kutembea na kushiriki shughuli nyingine za kimasomo na kijamii.

Uongozi wa hospitali unawakaribisha wazazi na walezi kuwaleta watoto wenye mahitaji ili kupata matibabu na matibabu hayo yanatolewa kila sikul na huduma inatolewa kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 17/07/2026

HAKUNA KUSAFIRI TENA: HUDUMA YA KUSAFISHA DAMU (DIALYSIS) YATOLEWA HOMSO

17/07/2026

Rais wa Chama cha Himofilia Tanzania, anayo furaha nyote kwenye ufunguzi wa kliniki ya himofilia mnamo tarehe 21 Julai katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea.

Ufunguzi wa kliniki hiyo ni hatua muhimu ya kuleta huduma karibu zaidi kwa wagonjwa wa himofilia mkoani Ruvuma na mikoa ya jirani.

Katika ufunguzi huo, kutakuwa na UPIMAJI BURE kwa wagonjwa wapya pamoja na utoaji wa elimu kuhusu utambuzi, utunzaji na matibabu ya ugonjwa wa himofilia. Huduma hiyo inalenga kuwafikia watu wengi zaidi na kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu mapema.

K**a una mtoto au ndugu mwenye changamoto za kuvuja damu kwa muda mrefu, fika siku hii kwa msaada zaidi. Kutambua tatizo mapema

Upimaji wa Himofilia: Hatua ya kwanza kuelekea matibabu.

Photos from Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Songea's post 17/07/2026

WAGONJWA 58 WAFANYIWA UPANDIKIZAJI WA FIGO KWA MAFANIKIO

Huduma za afya za kibingwa zimepiga hatua baada ya Serikali kuhimiza Watanzania na wadau kuchangia Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto, ili kuokoa maisha ya wagonjwa wasioweza kugharamia matibabu hayo.

Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha iliyofanyika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb), mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema dhamira ya Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tiba za kibingwa, mafunzo, tafiti na utalii wa matibabu katika Afrika Mashariki na Kati.

Takwimu zinaonesha mafanikio makubwa tayari yamepatikana: wagonjwa 58 wamefanyiwa upandikizaji wa figo kwa mafanikio, huku watoto 31 wenye selimundu wakipandikizwa uloto, matibabu yaliyokuwa yakifuatwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, Hospitali ya Benjamin Mkapa sasa inatoa huduma za ubingwa 20 na ubingwa bobezi 17, hatua iliyosaidia kuokoa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yakitumika kwa rufaa za nje.

Serikali pia imeanza ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji wa Figo kwa ushirikiano na TOKUSHUKAI Medical Corporation ya Japan, pamoja na maandalizi ya Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji wa Uloto.

Want your business to be the top-listed Health & Beauty Business in Songea?
Click here to claim your Sponsored Listing.

Category

Address

P. O. BOX 5
Songea