Simulizi Za Gilbert
Officialy Page ya Simulizi na Riwaya za mwandishi wako Gilbert Evarist Mushi. WhatsApp +255765824715
23/04/2026
Kutoka kwa Mwandishi Halfani Sudy ✍️✍️
Kitabu changu cha saba ni Sanduku Jeusi..
Sanduku Jeusi kinaungana na vitabu vyangu sita nilivyovitoa kwa nyakati tofauti.
1. Penzi Chungu.
2. Farida
3. Kipepeo Mwekundu
4. Kanda ya Siri
5. Msako Hatari
6. Kirusi Kipya
Na sasa ni Sanduku Jeusi.
Sanduku Jeusi kitakufikia popote ulipo nchini Tanzania.
Ni hivi karibuni.
Usipange kukikosa!
15/04/2026
Halfani Sudy
Mwandishi wa riwaya za kiswahili za kipelelezi na kijasusi Tanzania na Afrika ya Mashariki.
"Ahsante Mwenyezi Mungu kwa kipaji hiki..." Halfani Sudy anasema.
Mswaada wake wa riwaya ya Mnara wa Posta umeshika nafasi ya pili katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandihi bunifu hapo jana Jijini Dar es salaam
Hii ni hatua nyingine kubwa katika maisha yake ya uandishi wa riwaya, baada ya ile ya mwaka 2021 kushika nafasi ya kwanza katika Tuzo za Safal Kiswahili Prize for African Literature kupitia mswaada wake wa riwaya ya Kirusi Kipya (mtoto wa rais)...
Simulizi Za Gilbert inampa hongera na kumtakia kheri kwenye mwendelezo wake wa utunzi na uandishi.
Hebu tuandikie maoni yako hapa, unamkumbuka haswa katika riwaya ipi?
15/09/2025
Riwaya ya Kipelelezi: Eva wa Edeni
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone number : 0765824715
Sehemu ya 03
Ni saa mbili na nusu asubuhi, Bi Sandra na Bwana Henry wanapata chai taratibu huku kila mmoja mkono wake mmoja ukichezea simu yake ya mkononi. Bwana Henry yeye alikuwa akifwatilia mubashara kipindi cha mirindimo ya asubuhi kupitia TBConline katika mtandao wa youtube. Mada iliyokuwa ikijadiliwa ni kuhusiana na wimbi la upotevu wa watoto huku mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro ikiongoza.
Kwa upande wake Bi Sandra yeye alikuwa katika uwanja wa meseji akijibishana na mtu. Alikuwa ni mwingi wa hasira huku akichakata ujumbe wa maandishi kwa kasi huku vidole vikitetemeka.
"Madame, kuna mzigo wako umeletwa hapa" Birigitha alisimama pembeni ya bosi wake akiwa amebebelea kiboksi kidogo chenye maua kwa juu.
"Ni nani kakupatia?" Bi Sandra akauliza kwa mshangao huku akiweka simu mezani. Akapokea mzigo ule.
"Ni kijana mwendesha pikipiki, ameniambia yupo nje anakungoja k**a utakuwa na chochote cha kumweleza." Birigitha alijibu.
"Mwambie nakuja" akasema huku akikifungua kiboksi kile.
Looooh! Alikiangusha kiboksi kile chini, kidole kidogo cha mkononi kikatoka ndani ya kiboksi kile kikiwa kimefungwa pamoja na flashi ndogo.
Hakika aliogopa.
Bwana Henry haraka alitoka nje lakini hakumwona mtu yule aliyeleta kiboksi kile, na hapo wakakumbuka kosa walilolifanya hadi kutumiwa kidole cha mtoto wao. Hawakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kumpigia Afande Richard. Alimjuza kilichotokea
"Windo letu limefeli, tukutane tulipopaki gari." Afande Richard aliwataarifu polisi wenzake baada ya kupokea simu ya Bwana Henry.
Walielekea hadi nyumbani kwa Bwana Henry na kuwakuta yeye na mwenzie wameketi wakiwa na huzuni nyingi katika nyuso zao. Bwana Henry alimpa ishara Afande Richard aitazame flashi iliyoambatanishwa na kidole kile.
Akaichomeka kwenye runinga iliyokuwa ukutani pale sebuleni, na ndani ya flashi ile kulikuwa na video moja tu. Akaichezesha.
"Na haya ndiyo malipo ya kosa mlilolifanya. Ahsanteni, hadi wakati mwingine." yalikuwa ni maneno kutoka kwa mtu aliyevalia kinyago cha kuificha sura yake asiweze kufahamika. Nyuma ya mtu yule alionekana Kinje anayeugulia maumivu.
Bi Sandra alikuwa akibubujikwa na machozi. Ni nani asiyeujua uchungu wa mama kwa mwanaye? Hakika ilikuwa ni kasheshe.
_____________________
Siku tatu zilipita bila dalili ya watekaji kupiga simu. Afande Richard alijaribu kila namna kutafuta mawasiliano nao kupitia nambari ile waliyoitumia mwanzo lakini hakufanikiwa. Akajaribu hadi kwa wabobezi wa maswala ya kimtandao lakini bado hakufua dafu. Aliikatia tamaa kesi ile.
"Kuna mpelelezi mmoja aitwaye Daniel Mwaseba, nadhani ushawahi kusikia chochote kumhusu. Huyu mpelelezi anatokea idara ya usalama wa taifa, yupo mkoani kwetu kwa ziara maalum ya kitalii yeye na mke wake wakitarajia kuupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea hifadhi ya taifa ya Mkomanzi. Najaribu kufanya jitihada za kuushawishi uongozi wake watusaidie kutupatia huyu mpelelezi asaidiane nawe" Bwana Patrick Ndakidemi ambaye ni mkuu wa kituo cha polisi Kimaroroni, alikuwa akijadiliana na Afande Richard ofisini kwake.
Na kweli yakafanyika mawasiliano kati ya kituo chake cha polisi na idara ya usalama wa taifa makao makuu, akajuzwa kwamba Daniel Mwaseba yupo likizo hivyo k**a ataridhia bila ya shuruti likizo ikavunjwa basi atasaidiwa.
Daniel Mwaseba, kijana mtanashati na kipenzi cha watanzania wengi lakini adui wa watukutu na wasiofuata sheria za nchi. Kijana huyu alikuwa na mkewe Elizabeth Neville ndani ya gari aina ya Toyota Hilux maeneo ya Shanti Town mjini Moshi. Yalikuwa ni majira ya jioni na walikuwa wakitoka katika mgahawa mmoja wakirudi katika hoteli waliyofikia. Siku mbili kabla walifikia Kibo Palace Hotel wakitokea Kimara Dar es Salaam nyumbani kwao baada ya maazimio ya wawili hao punde tu baada ya kupatiwa likizo ya wiki tatu.
Wakiwa ndani ya gari simu yake ilitoa sauti ndogo ikiashiria kuingia kwa taarifa. Akamtaka mkewe amsaidie kuiangalia huku akiitoa mfukoni simu hiyo na kumkabidhi kwani yeye alikuwa bize na usukani wa gari akiendesha.
"Daniel ni ujumbe kutoka kwa Chifu." Elizabeth alisema punde tu baada ya kuufungua ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa.
"Mmh! Anataka nini tena na wamenipa likizo?" Daniel alihamaki huku akizidisha umakini barabarani.
"Anasema ufungue upande wa barua Pepe kuna jambo amekutumia huko" Elizabeth Neville alisema huku akiwasha data na kuelekea katika upande wa barua pepe. Na hapo aliweza kuona taarifa hiyo.
Alimsomea. Yalikuwa ni maombi kwa Daniel kutoka kituo cha polisi cha Kimaroroni. Punde simu kutoka kwa chifu iliita.
"Ipokee, weka sauti ya juu." Daniel alisema.
"Habari yako kijana wangu Daniel," Chifu Abdallah Ntenga ambaye ni mkurugenzi idara ya usalama wa taifa alimsabahi Daniel
"Salama chifu, shkamoo. kuna mpya gani huko?"
"Marhaba Daniel. Bila shaka hiyo barua umeipitia. Ni jukumu lako kuwakubalia ama kuwakatalia maana sisi tunajua kwamba upo likizo hivyo hatuna uwezo wa kukulazimisha. Nikutakie jioni njema"
"Ahsante sana chifu. Jioni njema pia"
Waliagana, simu ikakatwa. Daniel na mkewe wakashauriana kisha wakakubaliana kuelekea huko kituo cha polisi Kimaroroni kuwasikiliza hapo kesho mapema asubuhi.
Ombi kutoka kwa mkuu wake ni amri.
Na kweli palipopambazuka wakajiandaa na kuelekea huko. Wakaik**ata barabara ya Moshi - Arusha wakiwa ndani ya gari yao, walipofika KiboshoRoad wakachepuka kulia kuik**ata barabara ya kibosho na punde baada ya dakika kadhaa wakafika, na huko wakapokelewa na mkuu wa Kituo akiwa sambamba na Afande Richard. Baada ya majadiliano kwa kina Daniel akiwa sambamba na mkewe walikubali kuwasaidia sakata lile. Daniel akaomba kukabidhiwa faili lenye ripoti kamili inayoeleza kwa kina sakata la mauaji ya mwanafunzi Julieth na upotevu wa mwanafunzi Kinje.
Alikabidhiwa, akaipitia, akaridhika. Akawa tayari kwa uchunguzi kwa siku inayofuata mapema asubuhi.
Daniel atafanikiwa kubaini watekaji hao?
Usikose Sehemu ijayo hapahapa 😊
ITAENDELEA
10/09/2025
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.
Msimu wa Kwanza. Sehemu ya 05
"Kuna watu wanamfwatilia, Ni chipu ya kumwonyesha mahali alipo" Daniel alijibu baada ya kutazama, akaichukua na kutia katika mfuko wake. Dokta Yusha akamshangaa Daniel kwa kitendo cha kukitia mfukoni badala ya kuiharibu na kutupa, lakini Daniel alijua ni kitu gani anafanya
"Najua unashangaa kwanini hivi, ila kusudi langu ni kwamba k**a kuna watu wanamfwatilia endapo wakiona kifaa hiki kimezimika ghafla watahisi huyu mtu ametekwa. Nafanya hivi kuwapoteza maboya k**a watakuwa wanamfwatilia, muda ukifika nitakiharibu" Daniel Mwaseba alimweleza Dokta Yusha.
**********
Gilbert Mwaitika akiongozana na Elizabeth Neville walifika alipokuwa David na wenzake baada ya kupewa maelekezo kutoka kwa David mwenyewe. Walipofika waliwakuta kina David karibu na msitu uliopo pembezoni mwa kijiji kimoja kiitwacho Masama, mahali ambapo helikopta hiyo ililala usiku kabla ya ziara ya rais kufanyika. David alikuwa ana fahamu lakini wenzake wawili walikuwa bado wangali usingizini.
"Nimejaribu kuwaamsha sana lakini hawajaamka, japo kupumua wanapumua" David alisema baada ya kupiga salute mbele ya Gilbert Mwaitika. Alimwona pia Gilbert Mwaitika akiwa ameambatana na mwanamke mmoja aliyevalia shati ya mikono mirefu yenye rangi ya samawati na suruali nyeusi. Alimtambua Gilbert Mwaitika kwa kuwa waliwahi kuungana pamoja kwenda kupambana na waasi nchini msumbiji mwaka mmoja uliopita. Lakini Mwanamke aliyeambatana na Gilbert Mwaitika, David hakumtambua wala hakuwahi kumwona hapo kabla.
"Vipi kwa upande wako upo sawa?" Gilbert Mwaitika alimuuliza David, baada ya David kujibu yupo fiti na hajapata mushkari yoyote basi Gilbert Mwaitika alimtambulisha David kwa Elizabeth Neville.
"David, kutana na Elizabeth Neville. Huyu ni askari mpelelezi kutoka idara ya usalama wa taifa"
"Habari Elizabeth Neville, mimi ndiye David, David Taiwan" David alijitambulisha huku akiupeleka mkono wake kwa Elizabeth Neville kumsalimu.
"Nafurahi kukufahamu David, tupo hapa kwa ajili ya kazi ngumu kidogo, kuwafahamu waliowafanya mshindwe kuirusha helikopta angani, na kuifwatilia pia helikopta inayoranda angani" alisema Elizabeth Neville huku akipiga saluti mbele ya David, mkono wa David ukabaki na mshangao baada ya Neville kutoupokea mkono ule na badala yake kuachia saluti
"Hii helikopta tutaitumia, David utasubiri hapahapa maana hawa nimeshawaitia gari ya dharura kutoka jeshini na itafika muda si mrefu kuwachukua wote" alisema Elizabeth Neville huku akiwatazama wanajeshi wawili waliolala chini huku wakionekana kuzidiwa na usingizi.
Gilbert Mwaitika aliitoa barakoa maalumu ya kuzuia hewa chafu katika mfuko wa suruali yake, akaivaa kisha akaisogelea helikopta ile na kuanza kuikagua. Wakati huo Elizabeth Neville alikuwa anamtazama David kwa macho ya kipelelezi, macho yake yalikuwa kazini muda huo. Alishaanza kumtilia shaka David, na alipomuambia kuhusu msaada utakaokuja muda mchache ujao haikuwa kweli, hakupiga simu sehemu yoyote kuita gari ya kuja kuwachukua kina David.
Alikuwa na sababu kufanya hivyo.
Baada ya kuikagua helikopta ile kwa takribani dakika kumi, Gilbert aliridhika. Yeye pamoja na Elizabeth Neville waliwaacha kina David pale chini wakisubiri gari ya wagonjwa k**a Elizabeth Neville alivyodai. Gilbert ndiye aliyekuwa rubani wa helikopta ile huku Elizabeth Neville akiwa pembeni yake, akiwa makini kutazama chini kila mahali kwa kutumia miwani ya shetani. Walizunguka angani zaidi ya mara tano lakini hawakuiona tena helikopta ile, walizunguka karibu mji wote wa Moshi lakini hawakuiona helikopta ile. Na hata mngurumo wake haukusikika tena.
Ilitoweka ghafla.
"Nadhani watu hawa kila hatua wapo karibu na sisi, haiwezekani tupaishe helikopta halafu ghafla wao watoweke, kuna mchezo hapa na inawezekana tunazungukana pia." alisema Elizabeth Neville
"Unahisi ni kina nani wanayafanya haya?" aliuliza Gilbert, akaweka umakini kumsikiliza Elizabeth huku akizidi kuiongoza helikopta ile,
"David na wenzake wawekwe chini ya ulinzi kwanza, wao wanaufahamu mchezo mzima"
"David? David huyu ambaye alizimishwa akasinzia asijue chochote?" Gilbert Mwaitika akamuuliza Elizabeth Neville kwa wakha mkubwa.
"Unadhani kuna mwingine zaidi ya huyu? K**a waliwekewa mtego wapate kusinzia wakati wanajiandaa kuirusha helikopta angani kwa nini yeye amewahi kuzinduka na wenzake bado hawajitambui? Lakini wote si makomandoo? Kwa kuwa wote ni wanajeshi basi k**a hiyo dawa ya usingizi iliyotegwa kwao iliwalevya wangelala wote watatu hadi sasa, na pia k**a ni kuzinduka wasingepishana sana. Ukijaribu kutazama hali halisi hivi sasa unaona David ni mzima kabisa, mwili wake hauonyeshi uchovu wowote ule. Lakini wenzake wawili wapo k**a wafu. Kwanini iwe hivyo?" alieleza Elizabeth Neville huku akiendelea kupepesa macho yake kila kona.
" Umeongea kitu kizito sana Elizabeth, japo kinaweza kuwa na ukweli ndani yake, lakini hatuna ushahidi wa kumhukumu David moja kwa moja"
"Kwa sasa watakuwa ni watuhumiwa nambari moja, tukijiridhisha na uchunguzi wetu kwamba hawana hatia basi tutamwachia yeye na wenzake, au wewe unaonaje?" alisema Elizabeth na kuachia swali kwa Gilbert.
Gilbert Mwaitika alijaribu kutafakari huku akiwa makini kuiongoza helikopta. Zilipita sekunde arobaini za ukimya huku sauti pekee za mngurumo wa helikopta yao zikisikika katika masikio yao
"Naungana na hisia zako Elizabeth, David tangu anapigiwa simu na jenerali tayari alikuwa anajitambua. Tutaamini vipi k**a ni kweli naye alitumbukia katika usingizi wa kifo k**a wenzake? Mpigie Chifu atume askari wa kwenda kumk**ata, tutaenda kumhoji tukiwa na Daniel pindi ziara ya rais itakapotamatika. Sisi tuendelee kuimarisha ulinzi angani" alisema Gilbert Mwaitika, palepale Elizabeth Neville aliwasiliana na Chifu kumweleza kila kitu. Chifu Abdallah naye akamshirikisha Jenerali Evance juu ya jambo lile, wote kwa pamoja wakaubariki mpango wa kumk**ata David na wenzake wawili.
*********
David alibaki palepale alipoachwa na kina Elizabeth Neville. Pembeni yake wanajeshi wenzake wawili walikuwa bado usingizini wakiwa hawana dalili yoyote ya kuzinduka. Akiwa pale chini kwa mbali aliona magari mawili yakija walipo, akafurahi kuona msaada unakuja kwani alishaanza kuchoka kusubiri, lakini alitahamaki baada ya kuona gari zile kusimama mbali kidogo na pale walipo, wanajeshi watano waliovalia magwanda ya kijeshi wakateremka na kusogea kwa mwendo wa tahadhari wakiwa na bunduki zao mikononi.
"Wale wajinga wamenigundua nini!" David aliwaza huku akitafakari namna ya kuwakimbia wanajeshi wale.
-------------------
Kule ghorofani Dokta Yusha alikuwa akimalizia kuvichomoa visindano katika kifua cha mwanaume yule waliyemtambua k**a Ochewa Owechi k**a ambavyo hati ya kusafiria waliyoikuta katika koti lake ilivyoeleza. Alipomaliza zoezi lile alimtaka Daniel Mwaseba aubebe mzigo wake ili waelekee hospitali. Kwa umakini mkubwa walishuka na mwili ule bila kugundulika na mtu yoyote, isitoshe pia kwa bahati nzuri hoteli ile haikuwa na kamera za ulinzi ambazo zingeweza kuwarekodi.
Walikuwa wakishuka kwenye ngazi kutoka ghorofa namba nne na hatimaye waliifikia katika sakafu ya tatu ya ghorofa, kwa umakini mkubwa wakazik**ata tena ngazi zinazowapeleka hadi ghorofa namba mbili. Ndipo Daniel Mwaseba alipotumia mkono mmoja tu ambao ni wa kushoto kumshika vyema Ochewa Owechi katika bega lake la kulia huku mkono wa kulia ukipambana kuitoa chipu ile iliyokuwa ikimwonyesha mahali Ochewa alipo. Alipoitoa mfukoni aliidondosha chini kwa makusudi. Chipu ile baada ya kudondoshwa chini ilianza kubiringika kutoka katika ngazi zile kuelekea ghorofa ya chini na kukwamia katika sakafu ya pili ya ghorofa, mbele kabisa ya mlango wa chumba cha kwanza cha ghorofa namba mbili, hatua chache kutoka ngazi ilipo. Maandishi ya juu katika mlango ule yalisomeka "EMERGENCY ROOM/ CHUMBA CHA DHARURA", na maandishi hayo yalikuwa yamepambwa kwa wino mwekundu.
ITAENDELEA
Riwaya hii ina Jumla ya Misimu mitano. Kila msimu ni Tshs 1000 tu. Ukilipia 3000 utaipata misimu yote. Lipa kwenda Mpesa namba 0765824715 kisha njoo whatsapp kwa namba hiyohiyo nikutumie
06/09/2025
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.
Msimu wa Kwanza. Sehemu ya 04
"Unaona pale aliposimama mkuu wa majeshi, Jenerali Evance? hebu nenda mfuate sasa hivi, kuna kijana atakuunganisha nae ili mfuatilie ile helikopta inayoranda angani"
"Sawa Chifu" Elizabeth Neville aliitika na palepale alielekea mahali alipo jenerali Evance.
Alimkuta jenerali Evance akiwa na kijana mmoja aliyevalia magwanda ya kijeshi, mrefu kiasi mwenye mwili wa mazoezi.
"Elizabeth Neville, kutana na Gilbert Mwaitika. Ni kijana wangu ninayemwamini na kumkubali sana. Mtashirikiana k**a alivyokuambia chifu, nadhani mnafahamu ni wapi pa kuanzia, mtafuteni David kwanza mtapata pa kuanzia." Jenerali Evance alisema, Elizabeth Neville na Gilbert Mwaitika walitazamana, wakasalimiana kwa ishara ya kupiga saluti
Upande wa pili alipo Chifu Abdallah Ntenga alionekana akiwasiliana na watu fulani kupitia kisikilizio alichokipachika sikioni. Alikuwa akiwasiliana na maofisa watatu kutoka idara anayoisimamia. Maofisa hao ambao walikuwa karibu sana na Mheshimiwa Rais wakimwekea ulinzi ni Gabriel, Godwin pamoja na Deusderi. Chifu aliwataka Maofisa hawa kumtazama mheshimiwa rais kwa karibu zaidi baada ya kuzuka kwa hali ya taharuki. Yote haya yalifanyika kimya kimya ili kuzuia hofu kwa wananchi na viongozi kwa ujumla ili ziara iweze kutamatika salama. Yote haya yalifanyika kwa weledi mkubwa chini ya usimamizi wa Chifu Abdallah Ntenga, mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa.
Wakati huohuo Mh Eliud Sumbi ambaye ni makamu wa rais alikuwa ametulia kitini akimtazama rais Mark aliyekuwa akizidi kuwahutubia wananchi. Mh Eliud Sumbi mbali na kutulia lakini alikuwa akijilaumu sana baada ya mpango wake kufeli, alipanga katika ziara hii aitumie kumsambaratisha waziri wa Ulinzi Dr Edward Bavu na alishamwandaa mtu maalumu wa kuifanya kazi hii. Alimleta nchini jasusi Ochewa Owechi kutoka nchini Kenya kwa gharama kubwa ili aje kuitenda kazi hii. Mheshimiwa Eliud Sumbi alimfahamu vyema Daniel Mwaseba. Alifahamu ni mtu ambaye hupenda sana kufukunyua mambo. Alipomwona Daniel Mwaseba akizungumza na Chifu na baadae kumwona tena Daniel akitazama upande wa Five Star hoteli aliona mpango wake unaelekea kufeli, alihisi wenda watu hawa wameshanusa harufu ya hatari. Alipomwona mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa akiteta na jenerali Evance aliona mambo yameshaharibika, ikambidi ahairishe mpango wake kwa kumtumia ujumbe Ochewa Owechi ili aweze kuondoka pale haraka. Hakuwa na shaka yoyote juu ya jasusi Ochewa Owechi, aliamini ujumbe aliomtumia kule ghorofani utakuwa umeshatekelezeka.
Lakini hakujua k**a Daniel alishafanya yake, hakujua k**a jasusi huyo kwa sasa yupo katika mikono ya Daniel Mwaseba
Kwa nini Mh Eliud Sumbi anataka kumuua Dr Edwin Bavu? Kuna lipi lililojificha? Ungana nami katika riwaya hii yenye visa vya ajabu, ni mimi mwandishi wako Gilbert Mushi.
*****
Ilimchukua dakika tano tu Dokta Yusha kufika juu ya ghorofa ile, na huko alimkuta Daniel Mwaseba amejiinamia pembeni ya mwili wa Jasusi yule.
"Ooh Mungu wangu! Ni sumu ya aina gani hii inamfanya mtu avimbe mwili mzima kiasi hiki? Sijui k**a atapona huyu labda nijaribu tuu lakini sijawahi kuona sumu k**a hii" alisema Dokta Yusha baada ya kusogea karibu. Alishangazwa na aina ya sumu iliyokuwa katika mwili wa mwanaume yule. Mwili wake ulivimba na kuwa mkubwa k**a unga wa ngano uliotiwa amira na kukandwa kisha kuanikwa juani. Daniel Mwaseba aliinua macho yake kumtazama Dokta Yusha.
"Angeniua huyu, ilinibidi nifanye hivi bwana Yusuph Shaweji" Daniel alisema huku akitaja jina kamili la Dokta Yusha. Dokta Yusha bila kuchelewa alikishusha kibegi chake na kukitua chini, akakifungua na kuvaa gloves
"Mvue nguo ya juu, natakka abaki kifua wazi" Dokta Yusha alimwambia Daniel, Daniel Mwaseba alianza kumvua mwanaume yule koti alilovalia, akamvua na tisheti aliyovalia, tisheti hiyo ilikuwa na picha ya fuvu la binadamu kwa mbele.
Dokta Yusha alitoa visindano vingi vidogovidogo na kuvisokomeza katika kifua cha mwanaume yule, akavisokomeza na visindano vingine katika bega, sehemu ambayo ngumi za Daniel zilitua.
"Nisaidie kupanua kinywa chake," Yusha alisema huku akivuta majimaji kutoka kwenye kichupa kidogo kwenda katika bomba la sindano.
Daniel Mwaseba akatii k**a alivyosema Dokta Yusha, akakipanua kinywa cha mwanaume yule,
"Mmh! Jamaa ana ulimi mweusi k**a wa Ng'ombe, cheki na meno yake," Daniel alisema baada ya kukipanua kinywa cha mwanaume yule.
"Hahaha, hujawahi kumwona mtu mwenye ulimi mweusi? Huwa inatokea, kuna hali fulani ya kibaiolojia inasababisha hivi, kwa wengine ni kutokana na vyakula, na hata maji pia. ila kwa huyu nadhani ni kutokana na mazoezi, anaonyesha amekomaa kimazoezi mno, hali inayonipa matumaini wenda mwili wake unaweza pia kupambana na sumu hii isimshambulie kwa kasi sana" Dokta Yusha akamwelezea Daniel, taratibu akalibinya bomba lile la sindano kuelekea katika kinywa cha mwanaume yule, matone matatu ya mji yakatua katika ulimi wa mwanaume huyo.
"Hii isipomsaidia hatutakuwa na ujanja mwingine tena Daniel, laiti angekuwa mchovu kiafya tungekuwa hatunaye tena huyu hadi sasa, baada ya dakika tano nitavitoa hivyo visindano kisha tutampeleka hospitalini angalau akabadilishiwe na damu maana hii sumu imetapakaa sana mwilini na kuichafua damu yake kwa kiwango kikubwa sana, tutafanya hivyo k**a hiki nachofanya hapa kitaleta dalili njema." alisema Dokta Yusha akimtazama Daniel. Daniel alibaki kumtazama tu bila kutia neno lolote, badala yake alisogelea brufcase ile iliyopo pembeni na kuifungua. Ndani aliona bunduki kubwa ya masafa marefu, miwani ya kumwezesha kuona mbali, pamoja na noti kadhaa za shilingi elfu kumi ya Tanzania. Akahamia katika koti la mwanaume yule, aliona paspoti. Akaikagua kwa makini
"Ni mkenya, jina lake ni Ochewa Owechi, umri wake ni miaka 43." Daniel alisema baada ya kuisoma paspoti ya mwanaume huyu.
"Sasa alikuwa na mpango wa kumpiga nani risasi?" Daniel alikuwa akijiuliza huku akizidi kukagua paspoti ile iliyoambatana na picha. Akaiweka paspoti ile katika mfuko wake. Akazipiga tena hatua hadi katika miguu ya mwanaume yule, akabonyea chini kidogo na kuvua buti zilizovaliwa na mwanaume huyo.
"Mmmh!" akaachia mguno huku mkono wake ukielekea puani kupambana kuidhibiti harufu nzito kutoka kwenye buti zile.
"Ona Daniel, angalia hicho kidude kimedondoka baada ya kumvua buti" alisema Dokta Yusha huku akielekeza mkono wake kilipo kidude hicho. Daniel akainama kidogo kukitazama.
"Kuna watu wanamfwatilia, Ni chipu ya kumwonyesha mahali alipo" Daniel alijibu baada ya kutazama, akaichukua na kutia katika mfuko wake. Dokta Yusha akamshangaa Daniel kwa kitendo cha kukitia mfukoni badala ya kuiharibu na kutupa, lakini Daniel alijua ni kitu gani anafanya
"Najua unashangaa kwanini hivi, ila kusudi langu ni kwamba k**a kuna watu wanamfwatilia endapo wakiona kifaa hiki kimezimika ghafla watahisi huyu mtu ametekwa. Nafanya hivi kuwapoteza maboya k**a watakuwa wanamfwatilia, muda ukifika nitakiharibu" Daniel Mwaseba alimweleza Dokta Yusha.
**********
Kwanini Makamu wa rais ana nia ya kumuua waziri wa ulimzi? Kuna nini nyuma ya pazia? Daniel atafanikiwa kupata chochote kwa mdunguaji aliyetiwa mikononi mwake?
ITAENDELEA KESHO
05/09/2025
Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.
Msimu wa Kwanza.
Sehemu ya 03
Daniel alipigwa na butwaa baada ya kushuhudia mwanaume huyo akiwa bado imara akizidi kumnyonga, mwanaume yule hata hakutetereka kutokana na kupigwa kisogoni na goti lake. Badala yake mwanaume huyo aliinyoosha shingo yake kuelekea kulia kisha kushoto huku mikono ikiendelea kuik**ata shingo. Daniel Mwaseba akizidi kunyongwa alikiri hii aliyokutana nayo ilikuwa ni anga nyeusi, kwa kuwa hakutegemea k**a mwanaume yule angestahimili uzito wa goti lake ambalo laiti likikupata k**a si kifo basi ni kulala usingizi unaofanana na kifo.
Katika mkono wa Daniel Mwaseba, kidoleni kulikuwa na pete ya shaba, pete ambayo aliinunua akiwa mapumzikoni nchini Ujerumani miaka miwili iliyopita, pete hiyo haikuwa pete ya kawaida k**a zilivyo pete nyingine. Pete hiyo ilikuwa ni silaha tosha kwa Daniel, silaha ambayo angeitumia k**a atakuwa katika mazingira magumu ya kutetea uhai wake, mazingira k**a haya anayokumbana nayo hivi sasa. Kwa kutumia kidole gumba aliikandamiza kwa nguvu pete ile aliyovalia katika kidole cha shahada, hapohapo ikajifyatua na sindano nyembamba ikajichomoza katika uso wa pete. Daniel akazikusanya nguvu zake katika mkono wa kulia uliovalia pete ile, akakunja ngumi yake na kuipeleka mara mbili mfululizo katika bega la jamaa. Jamaa aliendelea kumnyonga Daniel kwa sekunde tatu tu, sekunde ya nne jamaa alilegea na kumdondokea Daniel katika kifua chake, hapo Daniel akaanza kupambana kuivuta pumzi kwa fujo kwani ilibakia kidogo tu aende kuisalimu kuzimu.
"K**a isingekuwa hii pete leo ningekufa, inaonekana watu walio nyuma ya hili ni watu waliojipanga vyema" aliwaza Daniel huku akijitahidi kuvuta pumzi kwa shida. Ngumi mbili alizozipiga ziliishindilia pete katika bega na kupelekea sindano ile yenye sumu kumchoma jamaa.
"Sindano ina sumu kali sana, nisipofanya kitu jamaa atanifia hapa na sitapata chochote, hapaswi kufa hadi nijue katumwa na nani" Daniel aliwaza, haraka alitoa kichupa kidogo chenye maji ya rangi ya shaba katika mfuko wa koti lake, akaichana nguo ya jamaa pale begani alipokita pete ile. Aliona alama mbili zilizovimbia kwa matone madogo ya damu, alama ambazo bila shaka ni ile sindano ilipenyeza baada ya kupiga ngumi zile. Daniel akafungua kichupa kile na kudondoshea tone moja la maji yale ambayo yalikuwa ni maalumu kwa kupunguza kasi ya usambaaji wa sumu, kilichobaki ilikuwa ni yeye kumwaisha hospitalini ili kuuokoa uhai wake. Baada ya hapo alichomoa simu yake na kuitafuta namba ya daktari kutoka hospitali ya KCMC, alikuwa ni Dokta Yusha ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu.
Dokta Yusha alikuwa akitoka katika chumba cha upasuaji baada ya kudumu huko kwa takribani lisaa limoja, Dokta Yusha alikuwa ni mmoja kati ya madaktari wakubwa na maarufu katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi. Alikuwa akizipiga hatua zake kuelekea katika ofisi yake, ndipo katika mfuko wa koti lake alisikia simu yake ikitoa mtetemo kuashiria kuna mpigaji. Aliitoa na kutazama kwa makini, alipoitazama alimfahamu mpigaji ni nani, akaipokea na kuiweka katika sikio lake la kushoto..
"Dokta Yusha habari? Naomba msaada wako haraka, kuna mtu wa muhimu sana hapa amezidiwa na sumu, ndani ya dakika kumi zijazo atanifia. Ni wa muhimu sana dokta, njoo na vifaa hapa five Star hotel juu ghorofani kabisa" Daniel alisikika simuni, na simu ikakatwa.
Dokta Yusha alielewa. Palepale aliingia katika ofisi yake na kuchukua kibegi chenye baadhi ya vitu ambavyo aliviona vitamsaidia aendapo, bila kubadili vazi lake la kidaktari alielekea nje na kuchukua usafiri wake. Kutoka pale hospitalini hadi ilipo hoteli ilimchukua dakika sita tu kutokana na barabara kutokuwa na foleni yoyote.
*******
Taarifa ya kubadilishwa kwa helikopta ilionekana kumshtua sana jenerali Evance, hakuwa amepata taarifa yoyote kutoka kwa vijana wake tangu awakabidhi kazi ya kuimarisha usalama. Ni jana tu alitoka kuzungumza na vijana wake watatu aliowapendekeza katika kazi ya kuzunguka na helikopta angani, na leo aliona helikopta angani ikizungukazunguka hivyo akaamini ni vijana wake kiasi kwamba hakuwa tena na wazo la kuwasiliana nao.
"Hebu ngoja niwasiliane nao kwanza nijue kulikoni hadi wabadilishe helikopta bila kuniambia" alisema Jenerali Evance ambaye ni mkuu wa majeshi ya Tanzania, palepale alitafuta namba ya kijana mmojawapo kati ya watatu aliowapa kazi hiyo. Alimpigia David. Simu iliita na baada ya sekunde tano ikapokelewa
"David mmefanya kitu gani na wala hamsemi? Kwanini mmebadili helikopta bila kutoa taarifa? Upumbavu gani huu mnafanya kinyume na utaratibu?" jenerali Evance alianza kufoka kwa ghadhabu baada ya simu ile kupokelewa
"Mkuu hata sielewi ni kitu gani kimetokea, tulipoingia ndani ya helikopta ili tuweze kuiwasha ilitokea hali ambayo hata siielewi, mimi na wenzangu wawili tulipitiwa ghalfa na usingizi mkuu, ndio kwanza nimetoka katika usingizi mzito mkuu. Wenzangu bado hawajazinduka, nimejaribu kuwaamsha lakini hawaonyeshi dalili ya kuamka kabisa, nahisi kuna mtu ametuchezea mchezo," David alieleza simuni
"Unasema nini! Ooh shiit..... Ina maana hii helikopta inayoranda angani sio nyie?" Jenerali Evance aliuliza kwa kuhamaki, Upande wa Chifu Abdallah hali haikuwa nzuri hata kidogo. Kitendo cha Evance kuuliza maswali kwa namna ya mshangao alibaini kwa sasa mambo hayapo sawa kabisa, na huu ulikuwa ni mwiba mchungu sana kwake na katika idara yake. Alimsogelea jenerali Evance apate kusikia maongezi yale kwa ukaribu zaidi
"Kuna hatari hapa, hii sehemu si salama kwa Rais wetu. ndio kwanza vijana wangu wanatoka katika usingizi wa kifo baada ya kusinzia ghafla wakati wakijiandaa kupanda helikopta, bila shaka walifanyiwa mchezo walipotaka kuiwasha helikopta" jenerali Evance alimwambia Chifu Abdallah, palepale alipiga hatua kuondoka lakini ghafla alishikwa mkono na Chifu Abdallah.
"Wewe ni mtu imara, hatupaswi kukurupuka katika hili. Tutume vijana wafuatilie ni nani yupo nyuma ya hili, hivi sasa napozungumza na wewe tayari vijana wangu wapo kazini kimyakimya kufuatilia nani ana nia ya kuvuruga ziara hii." aliongea Chifu Abdallah baada ya kumshika jenerali Evance mkono
"Hii ni hatari Bwana Abdallah, endapo likitokea la kutokea hapa sisi ndio tutatazamwa, lazima tufanye kitu" Jenerali Evance akamwambia Chifu Abdallah
"Nawaamini vijana wangu, muda si mrefu watanipa majibu mazuri, wewe tafuta kijana wako mmoja aungane na kijana wangu ili wafuatilie nani amefanya hili hadi hao vijana washindwe kupaisha helikopta angani, na hiyo iliyopo juu angani ifuatiliwe na wahusika wak**atwe"
Maneno ya Chifu Abdallah yakamtuliza Jenerali Evance kwa kiasi fulani, akachukua ushauri ule na palepale akaitoa simu yake kuisaka namba ya kijana wake mwingine anayemtumaini sana.
"Ngoja nimwite kijana wangu yupo hapahapa ziarani, naomba ashirikiane na kijana wako ili zoezi liende haraka. Huyu kijana wangu yeye ni mzuri sana kwa mapambano kuliko upelelezi, ni miongoni mwa wanajeshi waliorudi salama baada ya kumalizika kwa vita nchini Afrika ya Kati, kwa kuwa vijana wako ni hodari katika upelelezi naomba umuunganishe na vijana wako ili nguvu iongezeke, ninamwamini sana" Jenerali Evance anamwambia Chifu kwa unyenyekevu mkubwa.
"Ataambatana na Elizabeth Neville waifuatilie helikopta ile, mtaarifu aje sasa hivi maana mambo yanaweza kuharibika k**a tutazidi kuchelewa"
Palepale Jenerali Evance anampigia Gilbert Mwaitika, ambaye ni mmoja kati ya wanajeshi hodari sana katika vita. Gilbert Mwaitika ni mtaalamu wa mapambano ya ana kwa ana, ya kutumia silaha, na hata ya mbinu za kikomandoo. Miaka kadhaa iliyopita mwanajeshi huyu alishiriki vyema katika misheni iliyoitwa Biashara ya Watoto, iliyoandikwa katika majarida na mwandishi mmoja, katika misheni hiyo mwanajeshi huyu alionyesha ukomavu wa hali ya juu katika kupambana na watu waliokuwa wakifanya biashara hiyo, jambo lililompelekea apande chati kutoka upolisi hadi kuwa mwanajeshi komandoo baada ya kwenda mafunzoni nchini Iraq. Na huko ndipo alipokamilika na kuwa komando.
Jenerali Evance alimpatia maelekezo Gilbert Mwaitika ni wapi alipo ili aje. Wakati huo chifu naye alimfuata Elizabeth Neville na kumpatia kazi mpya.
"Unaona pale aliposimama mkuu wa majeshi, Jenerali Evance? hebu nenda mfuate sasa hivi, kuna kijana atakuunganisha nae ili mfuatilie ile helikopta inayoranda angani" Chifu alimwambia Elizabeth Neville.
ITAENDELEA
Kina Daniel watafanikiwa kujua chochote? Vipi kuhusu Helikopta inayoranda angani Elizabeth Neville na Gilbert Mwaitika watafanikiwa kuinasa? Ungana nami katika sehemu ijayo hapahapa. Riwaya hii ina Jumla ya Misimu Mitano. Msimu wa Kwanza sasa upo tayari, Ni kwa Tshs 1000 tu unaweza kuupata. Lipa kwenda M pesa namba 0765824715 kisha njoo WhatsApp kwa namba 0765824715 nikutumie. Ukilipia 3000 utapata riwaya yote.
Click here to claim your Sponsored Listing.